Unaweza Kuyashinda Magonjwa Na Dhambi Kupitia Nguvu Za Mungu
Amini Sana Nguvu Za Mungu
Hebu tufungue kitabu cha Yoshua, sura ya 11. Miaka iliyopita, mara nyingi nimekuwa nikijifunza kuhusu watu wa Israeli na jinsi gani walivyoingia katika nchi ya Kanaani. Niliona usambamba wa watu wa Mungu katika siku hizi za mwisho na kuingia kwao katika Kanaani ya Mbinguni.
Nilijifunza kuachiliwa kwao kutoka utumwani Misri na kuchelewa nyikani. Niliona ulinganifu wa kutolewa kwa Watu wa Mungu kutoka Babeli na kuchelewa kwao nyikani. Niliona uzoefu wa Waisraeli wa kupanda na kushuka na wangapi kati yao waliokufa nyikani. Kisha nimejifunza jinsi walivyopita katika mto Yordani na pia njia yao karibu na Edomu, ambayo tena ilikuwa hadithi ya kuvutia.
Ningependa kuendeleza hadithi ambayo kwa sehemu fulani hatujazingatia sana, lakini ambayo inatuhusu sisi leo, na hiyo ndiyo sehemu inayopatikana katika kitabu cha Yoshua.
Sura chache za kwanza zinahusu zaidi ushindi wa mji mkuu ambao ulikuwa Yeriko. Kisha hadithi inakwenda kwenye ushindi wa Ai, kipindi muhimu sana. Kisha unakuja ushindi na hadithi zingine zaidi ambazo zimejaa mafunzo yanayo tuhusu sis leo.
Wacha tuanze na Yoshua 11 ambayo inaanza kuripoti vita. Wakanaani hawakukata tamaa kwa urahisi licha ya kushindwa kwa Yeriko. Kulikuwa na mfalme aitwaye Yabini ambaye aliazimia kuwakusanya Wakanaani wote dhidi ya Israeli.
"Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu, na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi tambarare za Dori upande wa magharibi, na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa. Nao wakatoka nje, wao na mjeshi yao yote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana. Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli." (Angalia Yoshua 11:1-5)
Hadi wakati huo Israeli ilikuwa haijawahi kukutana na jeshi kubwa kama hilo. Ilikuwa changamoto ya kweli kwa imani yao. Jeshi hili halikuwa kubwa tu, bali lilikuwa na silaha bora kuliko Israeli. Inasema katika mstari wa 4, “...na farasi na magari mengi sana.”
Farasi Na Magari
Wakati huo farasi na magari ya vita yaliwapa faida kabisa wamiliki wao. Wamisri walikuwa wameendeleza matumizi ya farasi na magari ya kukokotwa, ambayo yaliifanya kuwa serikali bora katika ulimwengu wa siku zao. Baadaye, nguvu zao za kijeshi ziliangamizwa kwenye Bahari ya Shamu.
Unajua habari ya jinsi walivyowafuata Waisraeli, kisha magurudumu yao yakakwama kwenye matope, na hatimaye maji yakawapiga na kuharibu kila kitu. Kilichobaki ni silaha juu ya maiti za wale waliotupwa ufukweni, na Waisraeli wakachukua na kuyamiliki. Basi hapo ndipo zilitoka silaha za Waisraeli
Hadi wakati huo katika historia yao, Israeli walikuwa hawajapigana kamwe vita na mtu yeyote. Lakini sasa walikuwa na silaha za Wamisri, ingawa hawakuwa na farasi na magari yao yoyote ambayo yalikuwa yameharibiwa.
Mungu alikuwa amewaambia kwamba hawapaswi kuwa na farasi wala magari ya vita. Hii haikuwa na uhusiano wowote na ukweli kwamba hawakuwa nayo, bali bado walikuwa na wakati au fursa hadi muda huo.
Kwa hivyo walikuwa na shughuli nyingi za kuteka ardhi huku jeshi hili kubwa lenye farasi na magari ya vita lilipokuwa likipangwa dhidi yao. Jeshi hilo lilikuwa na faida kubwa. Leo unaweza kulilinganisha na jeshi lenye vifaru, huku jeshi dogo la Israeli likiwa na magari kama jeep za kijeshi tu.
Angalia hapa katika kitabu cha Yoshua:
"BWANA akamwambia Yoshua, Wewe usiogope kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa wakiwa wameuawa wote mbele ya Israeli; utawakata farasi wao, na magari yao utayateketeza kwa moto. (Soma Yoshua 11:6).
Kwa kawaida jeshi la ushindi lingemiliki silaha hizo ili kujipa faida. Walikumbuka jinsi walivyochukua silaha kutoka kwa Wamisri waliokufa ufukweni. Waliona hiyo kama nyara za vita. Lakini sasa wao waliambiwa kuharibu nyara hizo.
"Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafla; wakawashambulia. BWANA akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza mpaka kufikia Sidoni ulio mkuu, tena hadi kufika Misrefoth-maimu, tena hata kufikia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawaua wote, wasibakize hata mtu mmoja Yoshua akawafanyia vile vile kama BWANA alivyomwamuru; akawakata farasi wao, na kuteketeza magari yao kwa moto. Yoshua akarudi wakati huo na kuutwaa Hazori, akampiga mfalme wa Hazori kwa upanga; kwa kuwa Hazori hapo awali ulikuwa ni kichwa cha falme hizo zote. 11Nao wakawapiga wote pia waliokuwamo ndani ya Hazori kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa; hakubakizwa hata mmoja akiwa hai; kisha akauteketeza Hazori kwa moto". (Angalia Yoshua 11:7-11).
Kisha inaendelea kuripoti zaidi ushindi wa Yoshua, lakini nataka kurudi nyuma pale kwenye uchomaji wa magari ya vita na kulemaza farasi na kuuliza:
"Je, Kwa nini Mungu aliamuru hivi?"
Mungu alikuwa tayari amewaambia wasichukue farasi na magari. Tunaweza kusoma kuhusu hili katika Kumbukumbu la Torati 17. Mstari huu unahusu mfalme wa baadaye ambaye hakuwepo wakati huo, lakini Mungu, alikuwa amesema wangetaka mfalme.
Baada ya ushindi wa Yoshua na nchi kugawanywa, yeye alijiondoa na hakuwa kiongozi tena na hakuwahi kuwa mfalme. Kila kabila lilikuwa na jukumu la kuwateka Wakanaani walioishi katika eneo lao. Vita havikuongozwa tena na jenerali mmoja tu.
Lakini acheni tuchunguze unabii wa Mungu kuhusu mfalme wa wakati ujao. Mungu alijua hawatabaki kama walivyokuwa na siku moja wangehitaji mfalme. Unajua hadithi kutoka 1 Samweli wakati watu walimwomba Samweli awape mfalme na wakakataa kutii maonyo yake dhidi ya mpango huo. Angalia hapa:
"Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako ukaimiliki, na kukaa humo; nawe utakaposema, Nitaweka mfalme juu yangu mfano wa mataifa yote yaliyo kandokando yangu." (Torati 17:14)
Hivyo ndivyo walivyosema. Ilionekana kama vile Mungu alitabiri. Lazima nijiulize, je watu waliotengeneza ombi hili hata walijua juu ya unabii huu kwamba walikuwa watimiza? Au labda waliijua na kulitumia kama uhalalishaji.
“usiache kumweka yule atakayechaguliwa na BWANA, Mungu wako, awe mfalme juu yako; umweke mmoja katika ndugu zako awe mfalme juu yako; usimtawaze mgeni juu yako, ambaye si ndugu yako. Ila asifanye farasi wake kuwa wengi, wala asiwarudishe watu Misri, ili apate kufanya farasi kuwa wengi; kwa kuwa BWANA amewaambia, Tangu sasa msirudie tena njia ile”. (Angalia Torati 17:15-16).
Kwa nini Mungu alilitenga hili kama jambo ambalo hawakupaswa kulifanya wao? Jibu linaweza kupatikana hapa:
“Sasa najua kuwa BWANA amwokoa masihi wake; Atamjibu toka mbingu zake takatifu, Kwa matendo makuu ya wokovu Ya mkono wake wa kulia. Hawa wanataja magari na hawa farasi, Lakini sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu.” (Angalia Zaburi 20:6-7)
Je, tunaweza kuhisi ni kwa nini Mungu alikuwa mwangalifu sana kuwaambia Israeli wasizidishe farasi walipopata mfalme? Ilikuwa ni kwa sababu yeyote aliye na farasi na magari mengi atawategemea wao.
Nilijiuliza kwa nini Mungu hakuwashauri Waisraeli wawe hata na pinde na mishale, au panga na mikuki, ambavyo ndivyo vilikuwa vitu walivyochukua kwa Wamisri. Ni wazi kwamba Mungu hakushughulika na matatizo ya Waisraeli kwa wakati mmoja. Aliwaongoza hatua kwa hatua. Alijua udhaifu wa watu wake, udhaifu wa wanadamu, na akawaongoza kadiri alivyoweza ili kuwasaidia. Yeye alikuwa akisema,"Msije mkafanya hivyo."
Daudi alikuwa mfalme wa kwanza kupata idadi ndogo ya farasi na magari.
“ Tena Daudi akampiga Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kujipatia tena mamlaka yake huko Mtoni. Daudi akampokonya wapanda farasi elfu moja na mia saba na askari waliokwenda kwa miguu elfu ishirini; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila farasi wa magari mia moja akawabakiza”. (Angalia 2 Samweli 8:4-5)
Aliwalemaza farasi kwa kuwakata mshipa kwa sababu hiyo ilikuwa ni mapenzi ya Mungu, ambaye alikuwa amesema mfalme asiongeze farasi. Yeye hakufanya hivi ili tu kuwa mkatili. Wafalme wa Israeli hawakupaswa kufanya matumizi ya farasi na magari katika vita. Lakini Daudi alibakiza mia moja na magari mia moja.
Mrithi wake, Sulemani, alipata magari mengi zaidi ya haya na akawa na nguvu kabisa katika maana ya kijeshi. Na wafalme ambao walikuja baada yake walikuwa na farasi wengi zaidi, hata zaidi ya baadhi ya washirika wao, na walikuwa wameendelea sana katika uwezo wao wa kijeshi kwa njia hii.
Inafurahisha jinsi hii iliendelea kukua hatua kwa hatua, Na ilianza na wachache na ikakua kutoka hapo. Na kama unavyojua, wafalme waliofuata pia walimtegemea Mungu kidogo na wakategemea zaidi nguvu zao za kijeshi.
Kumtegemea Mungu Au Mwili
Hebu tusome baadhi ya maandiko juu ya jambo hili. Jambo la kwanza ambalo linaweza kuja akilini mwako ni:
“BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.” (Angalia Yeremia 17:5)
Hilo limekuwa tatizo kubwa kwa watu wa Mungu. Na katika ushindi wote wa Israeli hilo lilikuwa tatizo lao. Tuliona hili wakati wa ushindi wa Ai wakati walipotegemea nguvu zao wenyewe. Wakati huo hawakuwa wametengana na Bwana moyoni kama vile, lakini kulikuwa na mbegu mbaya pale ambayo ilikua imechipua. Na walipopata mfalme, hiyo mbegu iliongezeka zaidi. Kwa kweli, Sulemani alinunua farasi na magari kutoka Misri. Hakuridhika na alichokuwa nacho na alitaka kununua mengine zaidi.
“BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA.” (Angalia Yeremia 17:5)
Tunaweza kusoma zaidi kuhusu hili, lakini ni sampuli tu hiyo inawakilisha kanuni nzima ya Biblia.
“Mfalme haokolewi kwa jeshi lake kubwa, Wala shujaa haokoki kwa kuwa na nguvu nyingi. Farasi hafai kitu kwa wokovu, Wala hamponyi mtu kwa wingi wa nguvu zake.” (Angalia Zaburi 33:16, 17).
Kazi Ya Umishonari Ya Matibabu
Sasa linakuja swali muhimu. Je, farasi na magari ya vita ni nini katika kipindi au nyakati hizi tulizo nazo leo?
Mungu, katika siku hizi za mwisho, anataka kufanya kazi hasa ya umishonari ya matibabu. Anataka kusaidia na kubariki watu leo kama vile Yesu alivyofanya alipozunguka huko na huko na watu waliponywa.
Na leo tunaweza kuona kwamba ulimwengu umetengeneza mifumo ya ulinzi, yaani, farasi na magari ya vita. Hii inaweza kuonekana dhahiri katika mfumo wa matibabu, lakini Mungu hataki sisi kutegemea haya. Hataki tupofushwe macho na mambo haya, lakini tambua kwamba msaada unatoka kwa Mungu Yeye peke yake.
Huu angalau ni uwiano mmoja kati ya zama zile na leo ambao ulinidhihirika sana kwangu. Unaweza kusoma aya hii njia:
"Hakuna daktari anayeokolewa na wingi wa ustadi wa dawa zake; daktari mzuri hawezi kujiokoa kupitia elimu yake kubwa. Vifaa au zana za kazi ni tumaini lisilokuwa na maana kabisa kwa ajili ya usalama wake; wala haitaweza kumkomboa yeyote kwa kutumia nguvu zake nyingi.”
Hivyo ndivyo Mungu anataka kutuambia kupitia matukio katika historia. Hivi ndivyo tunapaswa kuona ndani yake, haswa tunapokuwa tukizungumzia juu ya ushindi wa Kanaani. Lazima tuone ni nini kilichowaongoza watu, hatua kwa hatua, mbali na Mungu.
Tusome aya nyingine;
“Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao..” (Angalia Zaburi 44:1)
Maadui hawa ni nani leo? Jibu ni hili, maadui hawa ni dhambi na magonjwa. Hawa ndio maadui tunaopigana nao.
“Kupitia Wewe (Mungu) tutaangusha dhambi na magonjwa; kwa jina lako tutakanyaga vitu hivi viwili ambavyo vinatuinukia kila siku hasa katika nyakati hizi mbaya."
“Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hauwezi kuniokoa.” (Angalia Zaburi 44:6)
Hivyo ndivyo hasa Mungu alitaka kuwaambia Israeli wakati alipowazuia kutoka kwa farasi na magari. Hakuwataka kutegemea vifaa vya vita.
“Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa kutoka kwa watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha, Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele.” (Angalia Zaburi 44:7, 8)
Kuna maneno mengine ningependa kuyasoma.
“Wamtumainio BWANA ni kama mlima Sayuni, Ambao hautikisiki, wakaa milele. Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, Ndivyo BWANA anavyowazunguka watu wake, Tangu sasa na hata milele.” (Angalia Zaburi 125:1-2).
Hizi zote ni aya zinazoonyesha jinsi ilivyo muhimu katika uzoefu wetu kumtegemea Mungu katika kila jambo.
Daudi Na Goliath
Kwa hiyo tungeweza kusoma hadithi moja baada ya nyingine ambapo maadui wa Mungu walikusanyika pamoja, lakini simulizi moja la kuvutia sana ni kisa cha Daudi na Goliathi. Hii inaonyesha mifumo miwili inayokabiliana katika mapigano. Mfumo mmoja unategemea mkono wa nyama, na mwingine mkono wa Mungu. Matokeo ya vita hivi tumepewa ili sisi tuweze kuelewa maana ya kutegemea mkono wa nyama. Kabla ya Daudi kuingia vitani, kwa imani yake isiyoyumba, Waisraeli walitetemeka mbele ya Goliathi, kwa sababu hawakumtegemea Mungu kabisa. Hivyo na sisi, kama tusipomtegemea Mungu kabisa, tutakuwa dhaifu kuliko "maadui" zetu, ambao wengi wao ni "dhambi na magonjwa".
Andiko lingine lenye kuvutia ni:
“Asiye haki huufanya uso wake kuwa mgumu; Bali mtu mnyofu huzifikiri njia zake. Hapana hekima, wala ufahamu, Wala shauri, juu ya BWANA. Farasi huwekwa tayari kwa siku ya vita; Lakini BWANA ndiye aletaye wokovu.” (Angalia Mithali 21:29-31).
Sasa hebu tusome hii:
“Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali. Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi. Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima.” (Angalia Isaya 30:15-17).
Wadhaifu Kuliko Maadui Zetu
Tunahitaji kufahamu ukweli kwamba tunapotegemea mkono wa nyama, tunakuwa dhaifu kuliko adui zetu. Huo ni ukweli ambao hauwezi kuonekana kwa haraka. Inaweza kuonekana hivyo tukitegemea farasi na magari tutapata faida.
Israeli waliogopa sana farasi na magari ya adui zao. Nchi ilipogawanywa, kabila la Efraimu lilitaka zaidi kuliko ilivyokuwa imetengwa, kwa hiyo waliambiwa wawashinde adui zao ili wapate zaidi, lakini wakawa na udhuru kwa sababu ya farasi na magari ya chuma ambayo adui zao walikuwa nayo. Walihisi kushindwa kabla hata hawajaanza.
Tunahitaji kujiuliza: Je, tunahisi tumeshindwa tayari? Kama ni hivyo, basi sio vyema. Hivi kweli nguvu zetu ziko wapi? Nguvu zetu zimo katika uongozi na uwezo wa Mungu kama inahusiana na kilimo, duka la chakula cha afya, kazi ya umishonari, au vita vyetu dhidi ya dhambi na magonjwa.
Utulivu Na Kujiamini
Tunachohitaji pia kuelewa hasa ni kwamba Njia za Mungu hazifanywi kwa ufahari mkubwa, wala hazifanywi kuwa imara kwa kuunganishwa na njia za kiulimwengu. Badala yake, Mungu anataka tufanye kazi kwa mshikamano. Anataka tufanye kazi kwa njia zisizo wazi na hivyo kutimiza mengi kwa sababu nguvu zitaonekana kuwa zinatoka kwake.
"Katika utulivu na ujasiri zitakuwa nguvu zako."
Hili ndilo lazima lifunuliwe. Kwahiyo ni moja ya masomo tunayoweza kupata kutoka kwenye kitabu cha Yoshua 11.
Kwa muhtasari, Wakanaani, maadui wa Israeli, walikusanya jeshi ili kuwashambulia Waisraeli, na Mungu akashinda ushindi bila farasi wala magari. Waisraeli walipoteka nyara, waliharibu magari ya vita na kuwalemaza farasi kwa kuwakata mshipa ili wasiweze kuchukua umiliki wao na badala yake wakaelekeza tegemeo lao kamili kwa Mungu.
Rafiki msomaji, Mungu akubariki sana, tutaendelea na makala yetu baadaye....................
Karibu kwa maswali na maoni yako.
Asante sana!
Comments
Post a Comment