Fahamu Sifa Za Nabii Wa Kweli

1. Nabii wa Kweli Hapendi Kujiita “nabii”!


Wale ambao wamebahatika kupata karama ya unabii huona kuwa ni vibaya kujiita jina hilo kwa sababu hupenda kumtukuza Mungu na sio kujitukuza wao wenyewe. Yohana Mbatizaji alikuwa nabii mkubwa kuliko manabii wote kama Yesu alivyosema:

Luka 7:26-28 “Lakini, mlitoka kwenda kuona nini? Nabii? Naam, nawaambia, na aliye zaidi ya nabii. 27 Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako. 28 Nami nawaambia, Katika wale waliozaliwa na wanawake hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.”



Hivyo, kulingana na Yesu, Yohana Mbatizaji alikuwa nabii, tena ni zaidi ya nabii.

Lakini Yohana Mbatizaji alipoulizwa wewe u nani? Hakujiita kwamba “mimi ni nabii”:

Yohana 1:19-21 “Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma

kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani? 20 Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. 21 Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La.” 

Kumbuka Yohana Mbatizaji alikuwa ni Eliya kweli na alikuwa ni nabii kweli,lakini hakusema “mimi ndiye Eliya na nabii”; kwa sababu kwa kujiita vivyo angejitukuza mwenyewe, majina hayo angeweza tu kuyaitwa na Yesu, alisubiri kutukuzwa na Mungu na sio kujitukuza mwenyewe. Hii ndiyo namna ileile ambayo Ellen White pia anatambulika kama nabii wa kweli, hakujitukuza mwenyewe, haukuwahi kujiita “nabii”! “Wakati wa majadiliano, nilisema kuwa sikudai kuwa ni nabii. Wengine walishangaa katika kauli hii, na kadri mengi yalivyosemwa kuhusu kauli hiyo, nitaitolea maelezo. Wengine wameniita nabii, lakini sijawahi kudhania jina hilo. Sikujisikia kwamba ni wajibu

wangu kujipa jina hilo mwenyewe. Wale ambao kwa ujasiri wanadhania kwamba wao ni manabii katika siku zetu hizi mara nyingi ni aibu kwa kazi ya Kristo. “Kazi yangu inajumuisha zaidi ya jina hili linavyoashiria. Ninajiona kama mjumbe, aliyepewa na Bwana jumbe kwa ajili ya watu wake” {Ellen G. White, Letter 55, 1905; imenukuliwa katika Selected Messages, book 1, pp. 35, 36}

Manabii wa kweli hawaoni kama ni jambo zuri kujiita jina hilo, wanamwachia

Mungu jukumu hilo. Sasa ni wengi kiasi gani duniani leo ambao wanajiita kuwa manabii? Ni zaidi ya maelfu, na kanuni hii moja tu inawafunua wazi wote kuwa ni manabii wa uongo. Wanajiita wenyewe kwamba ni “manabii”, na hiyo ni kwa ajili ya kujitukuza wenyewe, na sio kumtukuza Mungu.

2.  Nabii wa Kweli Ataishi Maisha ya Uongofu ya Kikristo.

Mathayo 7:15-16 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao.”

Njia nyingine ya kumtambua nabii kama ni wa kweli au ni wa uongo, ni matendoanayoyafanya katika maisha yake. Baadhi walishawishwa kumwamini Ellen White kama nabii wa kweli; kwa sababu ya jinsi alivyokuwa akiishi na kutenda. Tuna ushahidi ufuatao kuhusu maisha yake, na ushahidi mwingine unatoka kwa watu ambao sio Waadventista: “Alikuwa mwaminifu kabisa katika imani yake katika Funuo zake. Maisha yake yalikuwa yanastahili. Yeye hakuonyesha kiburi cha kiroho na hakutaka mapato ya aibu. Aliishi maisha na alifanya kazi ya nabii anayestahili.” {New York “Independent”, 1915}

“Maisha ya Bibi White yanapita maisha ya mtu yeyote ambaye nimewahi kumjua au ambaye nimekuwa nikihusiana naye, alikuwa mwenye kuvutia sana, mchangamfu na jasiri. Kamwe hakuwa mzembe, hakuwa mwepesi wa kunena haraka, au kwa njia yoyote mwepesi katika mazungumzo au namna ya maisha. Alikuwa ni mtu mwenye juhudi kubwa kuhusu mambo ya ufalme. Kamwe sijawahi kumwona akijivunia karama nzuri ambayo Mungu alimpa, au matokeo ya ajabu ya juhudi zake.” {A. G. Daniells, mtendakazi mwenza wa miaka mingi kwa miaka 23}

“Uzito wa ushahidi unaonyesha kabisa kwa uaminifu wa mashahidi wawili wa Ellen White – [ambao ni] maisha yake na huduma yake. Uaminifu wa tabia yake ulitambuliwa na watu wa siku zake, ikiwa ni Waadventista au la. Lengo kubwa la huduma yake katika kudhihirisha mvuto, ukweli, na nguvu za Yesu vilitambuliwa na wale walio ndani na nje ya kanisa lake. Jaribio lolote la kukubali aidha maisha yake bila huduma yake, au huduma yake bila maisha yake, linaonekana lisilo na maana. Kama Edward Heppenstall, anavyoiweka: “Haiwezekani kuweka thamani kubwa juu ya maisha yake na tabia na kuweka thamani ya chini juu ya maandiko yake.”” {WhiteEstate.org}

Gazeti la The Smithsonian magazine, November 17, 2014 lilimtaja Ellen G. White miongoni mwa “Waamerika 100 wa muhimu zaidi wa nyakati zote.” Mwanahistoria Randall Balmer alimwelezea Ellen G. White kama “mmoja wamifano ya muhimu zaidi katika historia ya dini ya Marekani.” { Balmer 2002, pp. 614–615.}.

 Hivyo maisha ya Ellen White yalikuwa yanastahili karama yake. Na kanuni hii ni mojawapo ya kuwatambua manabii wa uongo. Leo kuna manabii wa uongo wengi, baadhi yao hufanya hata biashara ya madawa ya kulevya, maisha yao wenyewe ndiyo hushuhudia kwamba ni manabii wa uongo. “Mti mbaya hauwezi kuzaa tunda jema.” Hivyo, wakati mtu anapojiita kuwa ni nabii, lakini hafanyi matendo kama ya Kristo, yuko katika orodha ya manabii wa uongo.

3. Nabii wa Kweli Atakemea Dhambi.

Kanuni hii pia ni ya muhimu kuwatambua manabii wa uongo, nabii wa kweli daima atakemea dhambi na uovu. Hii inawekwa wazi na Biblia katika mafungu yafuatayo:- Mika 3:8 “Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa roho ya Bwana; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake."

Yeremia 1:16 “Nami nitatamka hukumu zangu juu yao kwa habari ya uovu wao wote; kwa kuwa wameniacha mimi” Isaya 58:1 “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.”

Je! Ellen White alikemea dhambi? Yeyote ambaye amesoma maandiko ya Ellen White hawezi kukataa kwamba Ellen White alionyesha na kukemea dhambi. Aliandika vitabu kadhaa vinavyoitwa “Shuhuda kwa Kanisa” (Testimonies for the Church); ambavyo kwa hakika vinakemea dhambi na hukumu ya Mungu kwa wakosaji. Ellen White alikemea dhambi za ulimwengu na kuonyesha hukumu ya Mungu itakayokuja juu ya wale wote; ambao hawataki kuigeukia kweli, bali wanaendelea kujifurahisha katika udhalimu. Ellen White aliandika “dhambi lazima iitwe dhambi” na kwamba “hakuna dhambi inayopaswa kufunikwa kwa vazi la utakatifu”. “Katika kazi yetu, tunahitaji watu wa uhuru wa maadili, wasio na hatia na wasio na wasiwasi, ili kwamba wakati kanuni ya dini au wajibu inapokuwa katika hatari watasimama imara katika ulinzi wa ukweli. Tunahitaji watu ambao hawatakaa kimya wakati wanapoona maovu yakiingia na makosa yakifanyika. Tunahitaji watu ambao watakataa kutoa ridhaa kwa kuvikalia kimya vitendo visivyohaki. ” { E.G. White, Manuscript Releases, Vol.9, Letter 116, 1905}

Kukemea dhambi ni tunda la Roho Mtakatifu kama Yesu alivyoahidi:- Yohana 16:8 “Naye [Roho Mtakatifu] akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.” Manabii wa uongo hawakemei dhambi, bali huzificha na kuzisitiri; kwa sababu wao wenyewe pia wamo katika njia ileile.

4. Nabii wa Kweli Atamtukuza Mungu Pekee.

Marko 12:29-30 “Yesu akamjibu, [amri] Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; 30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.” Nabii wa kweli daima hatajitukuza mwenyewe, lakini badala yake atapeleka utukufu wote kwa Mungu. Ellen White kamwe hakuwahi kuonekana mahali popote akijisifu, au kujigamba kwa karama yake. Lakini wakati wote alimwinua Kristo juu na kumtegemea yeye kwa msaada wa kazi yote aliyoifanya katika maisha yake. Ellen White aliinua neno la Mungu mbele na juu kuliko mawazo yake mwenyewe. Ellen White kamwe hakujigamba kwamba yeye hawezi kukosa au kukosea, hakushawishi mtu kufuata maoni yake, isipokuwa aliinua Biblia na Yesu kuwa kanuni na mwongozo pekee wa mwanadamu. Soma jinsi alivyoandika mwenyewe:-

“Mfanye Kristo wa kwanza na wa mwisho na bora katika kila kitu. Daima mwangalie, na upendo wako kwa ajili yake kila siku utakuwa zaidi na wenye nguvu kadri unavyowasilishwa katika mtihani wa jaribio.” {E.G.White, Testimonies, Vol.7, P.46}

“Tunapaswa kukusanya kuhusu msalaba. Kristo yeye aliyesulubiwa lazima awe wazo la kutafakari, la mazungumzo, na la hisia zetu zenye furaha zaidi.” {E.G.White, Steps to Christ, P.103 – 104} “Kitu cha huduma zote ni kuondoa mbele ya macho swala la kujitegemea, na kumruhusu Kristo kuonekana. Kuinuliwa kwa Kristo ni ukweli mkubwa ambao wote wanaofanya kazi ya neno na mafundisho wanapaswa kudhihirisha.” {E.G.White, Manuscript Releases, Vol.16, P.295}

“Bwana anawataka ninyi mjifunze Biblia zenu. Hajawapa nuru yoyote ya ziada kuchukua nafasi ya neno lake. Nuru hii [huduma ya Ellen White] inapaswa kuleta mawazo yaliyochanganyikiwa kwenye Neno Lake, ambalo, kama litaliwa na kueleweka ni kama uhai wa nafsi.” {E.G.White, Selected Messages, book 3, p. 29}

Manabii wote wa uongo leo hii, hawamtukuzi Mungu wala neno lake. Unapoona nabii akijitukuza mwenyewe na kudai ana nguvu au uwezo, na wala hamtangulizi Yesu kwanza katika kila sifa na jambo; yeye ni nabii wa uongo. Ellen White alimtukuza Mungu Pekee, na hii inathibitisha kuwa ni nabii wa kweli.


5. Nabii wa Kweli Atafundisha Kwamba Kristo Alikuja Katika Mwili.

1 Yohana 4:2 “Katika hili mwamjua Roho wa Mungu; kila roho ikiriyo kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatokana na Mungu.” Je kuja katika mwili inamaanisha nini? Yohana 1:14 inasema Yesu alifanyika mwili akawa mmoja na sisi. Hii inaonyesha kuwa “kuja katika mwili” ni kuja katika asili ya kibinadamu, iliyo dhaifu na yenye kupendelea dhambi; lakini Yesu alishinda kwa njia ya kuuchanganya ubinadamu huo kwa uungu. Hivyo, nabii yeyote mwenye Roho ya kweli, atafundisha kwamba Yesu alikuwa na asili ya udhaifu kama yetu sisi, ila alitegemea nguvu za kiungu ili kushinda dhambi; na hii ndiyo namna ambayo Wakristo leo wanapaswa kuwa. Ellen White alifundisha ukweli huu:

“Asili ya ubinadamu ya Kristo ilikuwa kama ya kwetu.” {ST, Dec. 9, 1897, vol. 3, p. 436.} “Neno wa milele alikubali kufanyika mwili. Mungu akawa mwanadamu.” {ST, Feb. 20, 1893, vol. 3, p. 24}.

“Alijifanya mwenyewe kuwa hana utukufu, akatwaa juu yake namna ya mtumwa, na akafanyika katika mfano wa mwili ulio wa dhambi. Kwa ajili yetu akawa masikini, ili sisi kupitia umasikini wake tufanywe matajiri.” {ST, Feb. 20, 1893, vol. 3, p. 24} “Hakufanyika tu mwili, lakini alifanyika katika mwili ulio wa dhambi. Sifa zake za kiungu zilisitishwa kumtuliza uchungu wa nafsi yake au maumivu ya mwili wake.” {5BC 1124}.

 Hivyo, Ellen White alikuwa nabii wa kweli kabisa, alifundisha kuwa Yesu alikuja katika mwili, ulio wa dhambi, na ulioanguka kama wetu. Hivi ndivyo Biblia inafundisha: “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi. . . 17 Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake.” {Waebrania 2:14,17}. Manabii wote wa uongo, hawafundishi ukweli huu.


6. Nabii wa Kweli Atapokea Maono.

Sasa mtu hawezi kukamilika kuwa nabii, bila kupokea maono yoyote hadharani au sirini. Ellen White alipokea maono 200; mengine hadharani, na mengine sirini. Lakini, kwa namna gani, nabii wa kweli atapokea maono? Tunajifunza kutoka kwa nabii Danieli kwamba, wakati Danieli alipokuwa katika maono hakupumua kabisa: Danieli 10:17 “. . .Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu.”

_Hivyo, ni hakika kabisa kwamba, moja ya sifa za maono ya kweli, ni kwamba nabii wa kweli hatapumua kabisa wakati anapokuwa katika maono. Je! Ellen White hakupumua kabisa wakati wa maono yake?

_Tabibu mmoja anayeitwa Dokta Drummond, alidai kuwa maono ya Ellen White yalikuwa ni matokeo ya Uzugaji (Mesmerism au Hypnotism), lakini alipopata nafasi ya kumfanyia uchunguzi makini wakati wa maono, alisema “HAPUMUI”.

Wasiomwamini wangemziba pua zote na mdomo, na hata kuweka kioo mbele ya mdomo, lakini njia zote zilisibitisha kabisa kwamba Ellen White hakupumua katika maono.

“Tabibu mwingine anayeitwa Dk. Brown, alidai kwamba maono yake yalikuwa ni matokeo ya Umizimu (spiritualism), na kwamba angeweza kumdhibiti na kumwondoa kwenye maono, lakini alipopata nafasi ya kumfanyia uchunguzi wakati wa maono, alifadhaika na kusema “HAPUMUI”, huku akielekea mlangoni kutoka nje. Watu waliokuwa mlangoni wakamwambia: “Rudi nyuma, na ufanye kama ulivyosema kwamba ungeweza; kumwondoa mwanamke huyo kwenye maono”. Lakini Dokta, akiwa ametosheka kabisa, akashika kirungu cha mlango. Watu tena wakamwuuliza: “Dokta, vipi?” Dokta akajibu, “Mungu Pekee anajua!”

_Ushahidi mwingi wa watu waliotazama kwa macho, unathibitisha Ellen White

hakupumua kabisa wakati wa maono. Wakati mwingine ingemchukua masaa bila kupumua na bila kufa vilevile. Shetani hawezi kumzuia mtu kupumua kwa muda mrefu kiasi hicho bila kufa. Maono ya Ellen White yana sifa za maono ya kweli ya kutoka kwa Mungu. Danieli alipokea maono yake bila kupumua nayo yalikuja kutimia. Je! Maono ya Ellen White yalikuja kutimia pia?


7. Utabiri wa Nabii wa Kweli Utatimia.

Yeremia 28:9 “. . .neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa Bwana amemtuma kweli kweli.” Kumb. 18:22 “Atakaponena nabii kwa jina la Bwana, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena Bwana; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope.

_Hivyo, nabii anapotabiri kitu, na kitu hicho kikaja kutimia, basi nabii huyo ni nabii wa kweli asilimia 100. Katika maono 200 ya Ellen White, kuna tabiri nyingi amabazo zimekwisha kutimia, na nyingine zinatimia sasa. Hatutaweza kuziangalia zote, lakini tutachunguza hizi chache ili upate kuamini kwamba Ellen White kweli alikuwa nabii wa Mungu, na kwa usalama wako unapaswa kuamini maonyo aliyoyatoa.

LUTABIRI 1:

Katika ono moja, Ellen White alitabiri kuhusu vita kuu mbili za dunia, akisema:

“Nilionyeshwa wakazi wa dunia wakiwa katika machafuko makubwa sana. Kulikuwa na vita, damu, upungufu, ufukara, njaa na tauni, katika nchi. . . Usikivu wangu ndipo ulipoelekezwa kwenye tukio. Palionekana kuwa na muda mfupi wa amani. Ndipo tena wakazi wa dunia waliletwa mbele zangu, na kila kitu lilikuwa katika machafuko makubwa sana tena. Ugomvi, vita na damu, pamoja na njaa na tauni, vilipiga kila mahali. Mataifa mengine yalihusishwa katika machafuko na vita. Vita ilisababisha njaa. Upungufu na damu vilisababisha tauni. Na ndipo mioyo ya watu itashindwa kwa hofu, “na kwa kutafuta mambo ambayo yanakuja duniani.”” {RH, Aug. 27, 1861}.

_Maono haya Ellen White aliyatoa miaka 50 kabla ya vita ya kwanza ya dunia. Na

anasema kuwa vita ingetokea kati ya “wakazi wa dunia”, kisha pangekuwepo na “muda mfupi wa amani”, ndipo tena vita ingetokea tena kati ya “wakazi wa dunia” ikijumuisha mataifa mengine. Huu ulikuwa ni utabiri juu ya vita mbili kubwa za dunia kama inavyoonyeshwa hapo chini:_

Vita ya kwanza ya dunia (1914-1918).

Muda mfupi wa amani (1918-1939).

Vita ya pili ya dunia (1939-1945).

_Hivyo, utabiri huu wa Ellen White, ulitimia kikamilifu. Wote tunajua vita za kwanza na pili za dunia zilijumuisha dunia yote, pamoja na muda mfupi wa amani katikati; na ilikuwepo njaa na umwagaji damu, na vifo; kama Ellen White alivyotabiri._

UTABIRI 2:

_Ellen White alitabiri kuhusu vita ya kiraia ya Marekani; ambayo ilitokea miezi mitatu tu baada ya kuwa ameitabiri. Alitabiri kwamba:-_

“Hakuna mtu katika nyumba hii ambaye ameota kuhusu shida ambayo inakuja juu ya nchi hii. Watu wanafanya mzaha wa amri ya kujitenga ya South Carolina, lakini nimeonyeshwa kabisa kwamba idadi kubwa ya Majimbo yanaungana na Jimbo hilo, na kutakuwako na vita ya kutisha mno. Katika maono haya nimeona majeshi makubwa ya pande zote yakikusanyika katika uwanja wa vita. Nikasikia kuongezeka kwa kanuni, na kuona wafu na wanaokufa kila upande. Kisha nikawaona wakikimbia kwa haraka na kushiriki katika vita vya mkono kwa kila mmoja. Ndipo nikaona uwanja baada ya vita, wote umejaa wafu na wanaokufa. Kisha nikapelekwa hadi gerezani, na nikaona mateso ya wahitaji, ambao walikuwa wanamalizika. Ndipo nilipochukuliwa hadi kwenye nyumba ambazo zimepoteza waume, watoto au ndugu katika vita. Nikaona hapo msongo wa mawazo na uchungu.” . . .Kisha Ellen White akwaangalia wale waliokuwa pamoja naye chumbani na kusema. . . “Katika nyumba hii kuna ambao watapoteza wana wao kwenye vita hiyo.” {Remarks at Parkville, Michigan, January 31, 1893 – (General Conference Daily Bulletin., 2002, S. 37)}

_Vita ilitokea miezi mitatu tu baadaye, na kutimiza unabii huu kama Ellen White alivyokuwa ametabiri._

UTABIRI 3:

_Kwa miaka kadhaa, Ellen White alipokea maono kuhusu hukumu itakayokuja juu ya San Francisco. Lakini alikuwa na maono yake ya mwisho na ya kina kuhusu uharibifu wake Aprili 16, 1906. Akaona nyumba “zikitikisika kama mwanzi katika upepo” na majengo yakianguka chini._

“Kumbi za starehe, sinema, hoteli, na nyumba za matajiri zilitikiswa na kuvunjwa. Maisha ya watu wengi yaliangamizwa, na hewa ikajazwa na vimelea vya kujeruhiwa na hofu. Hofu ya matukio yaliyopitishwa mbele yangu siwezi kupata maneno ya kuyaelezea.” {Selected Messages, Book 3, P.40-41}.

_Ushahidi wa kihistoria unaonyesha kwamba siku mbili baadaye hapakuwa na ishara ya adhabu inayotarajiwa hadi saa 5:12 am. Wakati huo tetemeko lilitokea San Andreas lilipungua juu ya maili karibu 300, likivunja misingi ya mji. Kwa upande wake, tetemeko hilo liliacha miji 490 katika hali ya uharibifu wa jumla na watu zaidi ya 227,000 wasio na makazi, pamoja na zaidi ya 3000 waliokufa._


ELLEN WHITE KAMA MWANDISHI ALIYEVUVIWA WA AFYA.

_Jambo lingine linalothibitisha kwamba Ellen White ni nabii wa kweli, ni kazi yake ya uandishi wa afya; ambayo kwa wazi, imekuja kiajabu kama kazi ya Roho Mtakatifu kabisa. Lazima ijulikane kuwa Ellen White kamwe hakusoma shule yoyote rasmi, na aliachishwa shule kabla hajafikia ujana. Lakini, lazima pia ijulikane kuwa, Ellen White hakutumia kipimo chochote kugundua matatizo yaliyo katika vyakula na bidhaa mbalimbali. Ni ushahidi kwamba kazi yake ilikuwa ni kazi ya Roho Mtakatifu. Hapo chini hebu tuangalie mambo matatu aliyogundua kuhusu afya, na jinsi gani yalivyo ya kweli._


TUMBAKU.


Ellen White kuhusu madhara ya tumbaku, aliandika:

_“Tumbaku ni sumu ya polepole, ya udanganyifu, lakini mbaya sana. Kwa namna yoyote inavyotumiwa. . . ni hatari zaidi kwa sababu madhara yake ni ya polepole na kwa mara ya kwanza ni vigumu kuyatambua. Inasisimua na kisha hupoozesha mishipa. Inadhoofisha na kuharibu ubongo. Mara nyingi huathiri mishipa kwa njia ya nguvu zaidi kuliko vile inavyoweza kuathiriwa kwa unywaji wa pombe. Ni hila zaidi, na madhara yake ni vigumu kuondokana na mfumo. Matumizi yake huvutia kiu kwa ajili ya pombe na katika hali nyingi huweka msingi wa tabia ya pombe.” {Ministry of Healing, P.327.}._

Ellen White alitoa maelezo haya katika miaka ya 1860, wakati huo uvutaji wa sigara huko Marekani na maeneo mengine ya dunia, ilijulikana kama kitu cha faida kwenye afya. Haikuwa mpaka mwaka 1957, ndipo Chama cha Kansa cha Marekani kikasema kuwa uvutaji wa sigara unachangia sana katika ugonjwa wa Kansa ya mapafu. Hivyo Ellen White kwa kuvuviwa alijua madhara ya tumbaku tangu mapema kabla dunia haijagundua.

 

NYAMA.


_Ellen White aliandika kwamba Kansa ni “kijidudu”; ambacho mara nyingi husababishwa na ulaji wa vyakula dhaifu kama vile nyama za wanyama; ambao wanazidi kupata magonjwa:_

“Kama ulaji wa nyama ulikuwa na afya hapo nyuma, sio salama sasa. Kansa, vivimbe, na magonjwa ya mapafu kwa kiasi kikubwa husababishwa na ulaji wa nyama.” {Counsels on Health, P.133}. “Matabibu wa kidunia hawawezi kutoa ushahidi kwa ajili ya ongezeko la kasi la magonjwa kati ya wanadamu. Lakini tunajua kwamba mengi ya mateso haya yanasababishwa na ulaji wa nyama.” {Counsels on Diets and Foods, P.386}.

_Ellen White alifariki mwaka 1915, na haikuwa mpaka mwaka 1956 ndipo nadharia ya vijidudu ikathibitishwa na Dokta Wendell Stanley wa University of California. Leo mtaalamu yeyote wa afya, ambaye anajali vyakula, atakuambia wanyama wana magonjwa, na wamejaa madawa kiasi kwamba nyama zao sio salama tena kwa ajili ya chakula._

MAZIWA.

_Kuhusu maziwa Ellen White akiandika:_

“Nuru niliyopewa ni kwamba haitakuwa muda mrefu kabla hatujaacha vyakula vyovyote vya wanyama. Hata maziwa yatapaswa kuachwa. Magonjwa yanajikusanya kwa kasi kubwa. Laana ya Mungu iko juu ya nchi, kwa sababu mtu ameilaani.” {Counsels on Diet and Foods, P.357, (1899)}

_Daktari mmoja anayeitwa Robert Cohen, mwenye tovuti (notmilk.com), miongoni mwa madaktari wengine, pia anathibitisha madai ya Ellen White kwamba maziwa si salama kwa afya, Daktari Robert Cohen sio Mwadventista Msabato, lakini anakubali kwamba Ellen White alikuwa sawa. Anasema:-_

“Nina faida ya kutaja masomo ya kisayansi kutokana na masomo yaliyopimwa kwa usawa ili kufanya kazi kwenye safu zangu za kila siku. Ellen G. White “alijua” kabisa maziwa hayana uzuri wowote katika mwili. Maono yake yalikuwa yamevuviwa na Mungu.” {Robert Cohen, notmilk.com}

_“Kupitia kazi ya kuandika na kuzungumza ya umri wa miaka 70, Ellen White alizungumza juu ya uwazi. Kwa uzuri namna gani tunaweza kuchanganya ufahamu wake wa kidini na ushahidi wa kisayansi wa leo. Tunajua kwamba protini ya maziwa, na kasini, husababisha uzalishaji wa histamini. Baada ya kula jibini au ice cream, moja hutengeneza kamasi, na mengi ya hayo. Figo, kongosho, mapafu – vyote hujazwa na kamasi ya kunata. Kwa pamoja, mwili wa binadamu na viungo hupigwa na takribani 3-4 ya kamasi ambayo husababisha “ukungu wa ndani.”” {Robert Cohen, notmilk.com}._


MBEGU NA MBOGA.

 

_Ellen White kuhusu vyakula vya mbegu na mbogamboga aliandika:_

“Mbegu, matunda, karanga na mboga za majani ndivyo vyakula vilivyoteuliwa na Muumba wetu kwa ajili yetu. Vyakula hivi, vikiandaliwa katika namna rahisi na ya asili kama inavyowezekana, ni vya afya sana na vyenye lishe. Vinatoa nguvu, nguvu ya uvumilivu, na nguvu ya akili, vitu ambavyo havipatikani kwa chakula cha bei ghali Zaidi na vya kusisimua.” {Counsels on Diet and Foods, P.81}.

Dunia haifrahii vyakula hivi sana. Lakini utafiti wa kisayansi umegundua kuwa watu ambao hutumia vyakula kama hivyo huishi maisha marefu yenye afya (wastani wa miaka 10 zaidi) ukilinganisha na wale wanaokula vyakula vya nyama.

HITIMISHO

Kwamba Ellen White ni nabii wa kweli, ni kitu kisichokatalika kwa mtu yeyote aliye na moyo mnyoofu. Maandiko yake yana nguvu ya uvuvio wa Roho. Utafiti uliofanywa na kanisa la Waadventista Wasabato katika chuo kikuu cha Andrews University unahitimisha kuhusu uvuvio na athari za maandiko ya Ellen White kwa wote wanaoyasoma kwa moyo mnyoofu.

Waadventista “ambao mara kwa mara hujifunza maandiko ya Ellen White pia wana uwezekano mkubwa wa kuwa Wakristo wenye nguvu katika maisha yao ya kiroho na kwa uwakili wao kwa jamii zao kuliko washiriki wa kanisa ambao hawayasomi.” {Ministry, October 1982, p. 10}


Asomaye na afahamu .,...


Comments

Popular posts from this blog

Fahamu Mambo Yanayosababisha Uke Kulegea

Aina 9 Ya Vyakula Unavyopaswa Kuviepuka Unapokuwa Na Tatizo La Figo

Mambo 6 Yanayopelekea Mwanamke Kuhisi Maumivu Makali Anaposhiriki Tendo La Ndoa