Je Jumapili ni Sabato ya Wakristo?
Katika ukurasa huu natumaini kushiriki nawe baadhi ya mafungu ya Biblia ambayo yamechukuliwa nje na maana zake halisi ili kuonyesha kuwa Jumapili ni Sabato ya Kikristo. Mkristo wa kweli siku zote hataamini mawazo tu ya viongozi wa kanisa lake, lazima atafute kujua ukweli yeye mwenyewe kwa kufuatilia kama viongozi wake wako katika kweli au uongo. Fikiria kuhusu hili kwa muda, umeweka tumaini lako kwa kiongozi wako wa kanisa kana kwamba yeye hawezi kukosea, na kila anachokufundisha unaamini asilimia 100% na hautaki kuchunguza mwenyewe. Uko katika hatari kubwa!
Kama shetani akimuongoza huyo kiongozi wako katika njia ya upotofu, ataangusha kanisa zima la wale wanaomwangalia kiongozi huyo na kumwamini 100%. Na hiki ndicho kifaa cha shetani ambacho amefanikiwa kuweka watu katika mtego wake; kwa sababu anajua Wakristo wengi duniani wanawaangalia viongozi wao kana kwamba hawawezi kukosea katika kuhubiri ukweli wa Biblia, hivyo, juhudi zote za shetani ni kuwawinda viongozi awashike katika mtego wake, na akisha washika tu viongozi, anakuwa amewashika washiriki wote kwa maana ni kweli wakristo wengi wameweka macho yao kwa viongozi.
Na hii ndiyo sababu Yesu alikemea kuhusu kuwategemea viongozi vipofu, kwamba viongozi vipofu wakiwaongoza washiriki vipofu wote watatumbukia shimoni. Upofu aliomaanisha Yesu si upofu wa macho ya kimwili, bali ni upofu wa macho ya kiroho; yaani ile kushindwa kujua kwamba sisi kama wakristo tunapaswa kufanya nini huo ni upofu mkubwa. Na Je kama kiongozi hajui inampasa afanye nini, Je washiriki wote wanaomtegemea watajua? Hivyo, si vizuri kuwategemea viongozi.
Kama nilivyosema huko nyuma kwamba katika ukurasa huu tutaangalia baadhi ya mafungu yanayotumiwa na viongozi wa makanisa kuhubiri kuwa Jumapili ni sabato ya Wakristo, Na utakuja kuona kuwa mafungu hayo wameyatumia nje na maana zake.
…Fungu No. 1
Wakolosai 1:16 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato;”
Wahubiri wengi hulitikisa fungu hili lionekane kama linathibitisha kuwa Sabato ilipita, lakini Paulo katika fungu hilo hakumaanisha “Sabato ya wiki”, bali alimaanisha “sabato za mwaka”.
Katika Strong’s Exhaussive Concordance ya Biblia, neno Sabato la kiebrania linamaanisha vitu vifuatavyo…
‘Shabbath’ linalotamkwa, (‘shab-bawth’).
^
Linalomaanisha…
1) Sabato
1a) sabato
1b) siku ya upatanisho
1c) sabato ya mwaka
1d) sabato ya wiki
.
-Angalia Strong #07676
Nukuu hapa, Neno ‘Sabato’ la kigiriki lililotumika katika Wakolosai 2:16 ni ‘sabbaton’ (sab’-bat-on) linalomaanisha wingi; yaan, “sabato zaidi ya moja” au ‘siku za sabato’. Biblia ya kiingereza KJV imetaja kama “sabbath [days]”
Sabato zilizotajwa katika Wakolosai 2:16 siyo sabato ya wiki ambayo iko katika sheria 10 za Mungu. Ukisoma Walawi 23:23-38 utaona kuwa sabato zilizotajwa katika Wakolosai 2:16 ni “sabato za mwaka” ambazo zinajulikana kama “siku za sikukuu” zilizoadhimishwa kama kivuli kinachoonyesha kuwa katika siku za mbele Masihi angekuja kuwaokoa watu wake. Hii ndiyo maana Paulo anazitaja kama kivuli cha mambo yajayo.
Katika sabato hizo za mwaka ambazo ziliishia msalabani, desturi ilikuwa kama hivi: Siku ya 14 ya mwezi wa kwanza ilikuwa ni pasaka(Law 23:5), kisha siku ya 15 iliyofuata baada ya pasaka ilikuwa ni sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu ambayo ilifanyika kwa muda wa siku 7(Law 23:6). Katika siku ya 1 ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, ilikuwa ni sabato ambayo haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote isipokuwa ile ya kusongenza sadaka, pia katika siku ya 7 ya sikukuu hiyo haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote(Law 23:8).
Baada ya sikuku ya mikate isiyotiwa chachu kupita, siku ya pili baada ya Sabato walihesabu Sabato 7, tena zilipita siku 2 baada ya zile Sabato 7 kupita, walihesabu siku 50 mbele ambazo walitoa sadaka za vyakula na vinywaji na ilikuwa ni pumziko takatifu haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote(Law 23:9-21)
Harafu katika siku ya 1 ya mwezi wa 7 haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote, ilikuwa ni kusanyiko takatifu(Law 23:24-25), na katika siku ya 10 ya mwezi huo wa 7 ilikuwa ni siku ya upatanisho, haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote, ilikuwa ni sabato.
Walawi 23:27-32 “Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho;…Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho…Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.”
Harafu tena katika siku ya 15 ya mwezi huo wa 7 ilikuwa ni sikukuu ya vibanda iliyochukua muda wa siku 7, ambapo siku ya 1 haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote, na siku ya 8 baada ya sikukuu ya vibanda kuisha haikuruhusiwa kufanya kazi yoyote, ilikuwa ni sabato(Law 23:34-36). Hapa kitu cha muhimu kuzingatia ni kwamba, baada ya Mungu kutaja sikukuu zote hizo, katika Walawi 23:38 zile “siku za sikukuu” ambazo hakuruhusu kufanya kazi yoyote ndani yake, akaziita kuwa ni “Sabato za BWANA.” Hivyo, Sabato hizo ndizo zilizotajwa katika Wakolosai 2:16 na hazimaanishi sabato ya siku ya 7 ya kila wiki, kwa sababu ziliadhimishwa kwa kufuata tarehe maluumu na mwandamo wa mwezi kila mwaka. Kwa kifupi zinaitwa “sabato za mwaka.”
Hata hivyo huu sio ushahidi pekee, tukisoma katika Wakolosai 2:16 tunaona Paulo amezitaja “sabato” hizo kwa kuzijumlisha na “sikukuu”, “mwandamo wa mwezi”, na sadaka za “vyakula”, na “vinywaji” vile vile kama Walawi 23 inavyoweka wazi kuwa “sabato” hizo zilikuwa ndani ya “sikuku za Bwana,” na ziliadhimishwa kwa kufuata tarehe maalumu na “mwandamo wa mwezi,” na wakati wa sikukuu hizo wana wa Israeli walitoa sadaka za “vyakula” na “vinywaji.”
Wana wa Israeli waliadhimisha sikukuu hizo wakiaashiria kuwa Bwana aliwatoa katika nyumba ya utumwa Misri(Kut 12:17, 13:3), hivyo hii ilikuwa ni kivuli au mfano wa kwamba siku moja angekuja Masihi kuwaokoa watu wake kutoka kwenye utumwa wa dhambi. Na kwa kuwa Masihi mwenyewe alishakuja, hivyo haitakiwi kuziazimisha “sikukuu” hizo pamoja na “sabato” zake, na “mwandamo” wake, na “sadaka” zake za vyakula na vinywaji; kwa sababu Masihi ambaye sikukuu hizo zilionyesha kivuli chake alikuwa tayari ameshakuja Yeye Mwenyewe. Hiki ndicho alichomaanisha Paulo katika Wakolosai 2:16 pale aliposema kuwa “…mtu asiwahukumu ninyi(Wakristo) katika (sadaka za)vyakula au vinyinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo…” Lakini Paulo hakumaanisha sabato ya wiki, bali alimaanisha sabato za mwaka zilizofanyika kwa kufuata mwandamo wa mwezi katika zile sikukuu za wana wa Israeli.
Hata hivyo, hii sio njia pekee ya kuthibitisha kuwa sabato zilizotajwa katika Wakolosai 2:16 hazimaanishi sabato ya siku ya 7 ya kila wiki; kwa sababu kama Paulo kweli alimaanisha “sabato ya wiki” aliposema kuwa “…mtu asiwahukumu katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu, au mwandamo wa mwezi au sabato;” Kol 2:16. Hii ingemaanisha kwamba Wakolosai walikuwa hawatunzi ‘sabato ya wiki’ na hivyo angekuwepo mtu wa kuwalaumu kwa sababu hiyo. Lakini ukweli siyo hivyo, historia inathibitisha kuwa Wakristo wote wa mwanzo walishika ‘sabato ya wiki’ mpaka mwaka 325BK ambapo kanisa la Romani Katoliki lilibadilisha ‘sabato ya wiki’ kutoka Jumamosi kwenda Jumapili. Hivyo wakati Paulo anaandika walaka wake kwa Wakolosai Wakristo wote walikuwa bado wanatunza ‘sabato ya wiki’ na hivyo asingekuwepo mtu yeyote wa kuwahukumu kwa sababu ya ‘sabato ya wiki;’ maana wote pamoja na Paulo mwenyewe walikuwa wanaitunza ‘sabato ya wiki’.
Lakini ni kweli kwamba Wakolosai na Wakristo wengine wote wakati huo walikuwa hawatunzi sikukuu za kiyahudi pamoja na ‘sabato zake za mwaka’, na mwandamo wa mwezi, na sadaka zake za vinywaji na vyakula, hii ndio maana Wayahudi waliwahukumu Wakristo kwa sababu hiyo. Lakini siyo kwa sababu ya ‘sabato ya wiki’ kwa maana Wakristo wote walikuwa wanaitunza kama sheria ya 4 ya Mungu inavyowaamuru.
Hata hivyo, kama kweli Paulo katika Wakolosai 2:16 angekuwa anamaanisha sabato ya wiki ya siku ya 7, hii ingemfanya Paulo kujichanganya katika maneno yake pale alipowashauri Wakristo watunze sabato ya wiki. Hivyo, ukweli uko wazi kwamba Paulo katika Wakolosai 2:16 alimaanisha ‘sabato za mwaka’ za sikukuu, lakini kuhusu sabato ya wiki ya amri ya Mungu Paulo anasema…
Waebrania 4:4,8-11 “Kwa maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote;…Basi, imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.”
…Fungu No. 2
Hosea 2:11 “Tena nitaikomesha furaha yake yote, na sikukuu zake, na siku zake za mwandamo wa mwezi, na sabato zake, na makusanyiko yake yote yaliyoamuriwa.”
Ukweli rahisi ni kwamba sabato zilizotajwa hapo ni “sabato za mwaka” za sikukuu za Wayahudi zilizoorodheshwa katika Walawi 23:23:38. Hata hivyo ukiangalia katika Hosea 2:11 utaona imetaja pia mwandamo wa mwezi na sikukuu, vile vile kama Walawi 23 ilivyoelezea. Hivyo, sabato zilizokomeshwa ni “sabato za mwaka” zilizokuwa katika sikukuu za Wayahudi. Kwa hakika, Wakolosai 2:16 inathibitisha kuwa sabato hizo za mwaka zilikomeshwa, lakini siyo “sabato ya wiki” ambayo haihusiani na sikukuu, yenyewe ilianzishwa Edeni kabla wana wa Israeli hawajapewa sikukuu yoyote. Sabato ya wiki yenyewe haihusiani na sikukuu za Wayahudi, Mungu aliiweka tangu mwanzo wa kuumba kama ukumbusho wa matendo yake ya ajabu aliyofanya wakati wa uumbaji wa siku 6. Sabato ya wiki iliwekwa katika siku ya 7 ili kukumbuka uumbaji, na haihusiani na “sabato za mwaka” za sikukuu.
Hivyo kama mtu akisema Hosea 2:11, na Wakolosai 2:16 zinasema kuwa “sabato ya wiki” ni kivuli, na historia na Biblia vinathibitisha kuwa Paulo alitunza sabato ya wiki. Je Paulo naye alikuwa chini ya kivuli? Au kama baadhi ya watu wanavyosema kwamba kutunza sabato ya wiki ni kuwa chini ya sheria, na Paulo mwenyewe aliitunza. Je Paulo naye alikuwa chini ya sheria? Ukweli uko wazi Hosea 2:11 na Wakolosai 2:16 hazimaanishi “sabato ya wiki”, bali zinamaanisha “sabato za mwaka” za kwenye sikukuu za Wayahudi.
…Fungu No. 3
Wagalatia 4:9-11 “Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.”
Baadhi wanatangaza kuwa fungu hili linamaanisha “sabato ya wiki” eti kwa sababu ya neno “siku” lililotajwa hapo. Kama ukisoma kwa makini fungu hilo kuanzia Gal 4:8-11, utaona kuwa Paulo alikuwa anazungumzia Wagalatia ambao walitaka kuendelea na desturi na sherehe za kipagani kanisani. Pia Wayahudi wa Kikristo ambao walitaka kuendelea na sikukuu zilizoishia msalabani. Hakuna sehemu yoyote katika Wagalatia 4:8-11 ambayo inasema wazi kuwa Wakristo wasitunze sabato ya wiki.
Hata hivyo hii si njia pekee ya kuthibitisha kuwa Paulo hakumaanisha sabato ya wiki; kwa sababu kama kweli unaamini Paulo alimaanisha sabato ya wiki aliposema, “haipaswi kurudia kushika siku, na mwezi, na mwaka.” Hii ingemaanisha kuwa Wakristo wa wakati huo walikuwa hawashiki sabato ya wiki, na hivyo wangekuwepo wakristo wengine ambao walitaka kurudia kushika sabato ya wiki, na Paulo akawakataza kwamba hawapaswi kushika siku, lakini sio hivyo; kwa maana wakati huo Paulo alipowakataza Wagalatia kushika siku, mwezi, na mwaka yeye mwenyewe alikuwa anashika sabato ya wiki, pia Wakristo wote wakati huo walikuwa wanashika sabato ya wiki. Je inawezekanaje Paulo awakataze Wagalatia wasishike sabato ya wiki, wakati yeye mwenyewe alikuwa anashika sabato ya wiki maisha yake yote mpaka kufa? Ukweli uko wazi, Paulo alipowakataza Wagalatia kushika siku, mwezi, na mwaka, alimaanisha kwamba hawapaswi kushika sikukuu za Wayahudi, au sherehe za Wapagani, na wala sio sabato ya wiki.
Lakini kama kuna mtu ataendelea kubishi na kusema kwamba, “Paulo alipowakataza Wagalatia kushika siku, mwezi, na mwaka alimaanisha sabato ya wiki ya kwenye amri 10 za Mungu.” Naomba anielezee ni wapi katika amri 10 za Mungu anaona maneno “siku”, “mwezi”, na “mwaka”? Au ni wapi katika amri 10 anaona maneno “mwandamo wa mwezi”, “sikukuu”, “vyakula”, au “vinywaji”?
…Fungu No. 4
Warumi 14:5 “Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.”
Baadhi ya watu wanadai kwamba fungu hilo linamaanisha “siku ya kuabudu.” Karama ya Babeli ni “kuchanganyikiwa”, hii ndio maana makanisa yote ya Babeli wanadai kuwa fungu hilo linamaanisha “siku ya kuabudu.” Je huwezi kuona kuwa ikiwa mtu mwingine atapendezwa kufanya ibaada siku ya Jumamosi, mwingine Jumapili, mwingine Jumatano, mwingine Alhamisi, Je hayo siyo machafuko?
Tena cha kufurahisha zaidi hapa ni kwamba, wakati wa mtume Paulo hapakuwa na madhehebu mengi kama hivi leo, kwa mfano kimadhehebu tuchukulie palikuwa na dhehebu moja tu, hivyo kulingana na wahubiri Jumapili amri ya kanisa Katoliki wanaotumia Rum 14:5 kuthibitisha kuwa Sabato ilipita, wanamaanisha wazi wazi kana kwamba Paulo alisema, “mtu mwingine anapendezwa kufanya ibaada katika siku ya Jumatatu, mwingine Ijumaa, mwingine Jumamosi, mwingine sikuzote anatembea kwenda kanisani kufanya ibaada ya hadhara kivyake.”
Je ni vigumu sana kwa wale wanaotumia fungu hilo, kujua kwamba Paulo alimaanisha nini aliposema, “Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.”? Ukweli rahisi hapa Paulo alimaanisha “siku za sikukuu.” Kuna Wakristo waliokuwa wamezoea desturi za kiyahudi na za kipagani ambao walipendezwa kuendelea kushika siku za sikukuu na kula vyakula vilivyotolewa kwa sanamu. Kama ukisoma Rum 14 yote, utaona Paulo amesema hatupaswi kuwahukumu watu kama hao, maana Bwana anauwezo wa kuwainua.
Historia inathibitisha wazi kuwa Wakristo wote wa mwanzo walitunza sabato ya wiki hadi mwaka 325BK ambapo kanisa Katoliki lilianzisha Jumapili, hivyo wakati wa mtume Paulo hakuwepo mtu ambaye alipendezwa kufanya ibaada ya hadhara Jumapili, mwingine Jumamosi, kadri kila mtu anavyopenda. Bali walikuwepo watu ambao waliendelea kushika siku za sikukuu kama walivyopenda. Hivyo Rum 14:5 inamaanisha siku za sikukuu, wala si siku ya ibaada.
…Fungu No. 5
Matendo 20:7 “Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.”
Je unataka kusema hapo walikuwa wanafanya ibaada ya hadhara jumapili? Hapana! Kwanza mkutano huo ulifanyika wakati wa usiku, na ukisoma fungu linalofuata linasema, “Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika.” Mdo 20:8. Usiku huo kijana mmoja alizidiwa na usingizi akaanguka toka orofani (Mdo 20:9), tena walikuwa wakimega mkate na mkutano huo uliendelea mpaka alfajiri (Mdo 20:11). Je kwa sababu walikuwa wakimega mkate na ni siku ya kwanza ya juma, ndio inamaanisha sabato ilibadilishwa? Kwanza kumega mkate walikuwa wanamega siku zote bila kujali siku ya ibaada. Matendo 2:46 inasema, “Na siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba…” Kwa hiyo kumega mkate Jumapili haimaanishi kwamba ndio sabato ilihamishiwa Jumapili. Lakini kwa sababu wachungaji wanalitumia fungu hilo kudai kuwa ilikuwa ni huduma ya kanisa siku ya Jumapili, hivyo naomba walitendee haki fungu hilo la Matendo 20:7 kwa kufanya huduma ya ibaada usiku wa manane, mpaka alfajiri, na Kufanya huduma ya ibaada kila usiku wa manane.
…Fungu No. 6
1Wakorintho 16:2 “Siku ya kwanza ya juma kila mtu kwenu na aweke akiba kwake, kwa kadiri ya kufanikiwa kwake; ili kwamba michango isifanyike hapo nitakapokuja;”
Baadhi wanalitumia fungu hili kuhubiri kwamba sabato ilihamishwa kutoka siku ya 7(Jumamosi) hadi siku ya kwanza ya juma (Jumapili), eti kwa sababu Paulo anaagiza kila mtu kuweka akiba kwa ajili ya mchango. Tena hapo hakuna neno lolote linalosema wazi kwamba sabato ilibadilishwa kutoka Jumamosi kwenda Jumapili, lakini anachosema Paulo hapo ni kwamba “kila mtu aweke akiba kwake yeye mwenyewe” katika siku ya kwanza ya juma. Ili Paulo atakapofika usiwepo mchango; kwa sababu kila mtu atakuwa ameweka akiba kulingana na Mungu alivyomjalia. Hakuna sehemu yeyote hapo inayosema kwamba siku ya kwanza ya juma palikuwa na huduma ya ibaada kanisani, bali Paulo anasema kila mtu aweke akiba kwake kwa ajili ya changizo. Ukweli ambao wengi hushindwa kutambua ni kwamba hakuna Mkristo yeyote ambaye hakutunza sabato wakati wa mitume, Sabato ilibadilishwa na kanisa katoli katika karne ya 4, nyuma ya hapo hakuwepo hata mkristo mmoja aliyewahi kutunza sabato ya Jumapili.
…Fungu No. 7
Marko 2:23:28 “Ikawa alipokuwa akipita mashambani siku ya sabato, wanafunzi wake walianza kuendelea njiani wakivunja masuke. Mafarisayo wakamwambia, Tazama, mbona wanafanya lisilokuwa halali siku ya sabato? Akawaambia, Hamkusoma popote alivyofanya Daudi, alipokuwa ana haja, na kuona njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, zamani za kuhani mkuu Abiathari, akaila mikate ile ya Wonyesho, ambayo si halali kuliwa ila na makuhani, akawapa na wenziwe? Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato. Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia.”
Baadhi hudai sabato haina umuhimu tena kabisa; kwa maana wanasema Yesu aliivunja. Lakini ukweli hapa Yesu hakuvunja sabato, isipokuwa Wayahudi kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao walimzania Yesu kuwa amevunja sabato kwa kuwaacha wanafunzi wake wachume masuke ya ngano. Na hii ndiyo sababu Yesu aliwathibitishia Wayahudi kwamba Yeye wala wanafunzi wake hawakuvunja sabato, akamchukulia Daudi kama mfano; akasema, Daudi alipokuwa na njaa alienda kuchukua mikate ambayo ilikuwa hairuhusiwi kuliwa na mtu yo yote ispokuwa makuhani pekee, akaila kisha akawapa na wenzake. Hivyo, Yesu alisema, walichofanya wanafunzi wake ilikuwa ni ruhusa kufanywa siku ya sabato, wala hawakuvunja sabato. Dhambi ni uvunjaji wa sheria za Mungu (1Yohana 3:3), hivyo kama ukisema Yesu alivunja sabato unamaanisha kuwa Yesu alifanya dhambi, lakini Yesu mwenyewe hakufanya dhambi, wala hana doa, hivyo hakuvunja sabato.
Wayahudi walikuwa ni vipofu, hawakujua ya kuwa Yesu alikuwa anatenda haki siku ya sabato alipowaponya wagonjwa au alipowaruhusu wanafunzi wake kuchuma masuke ya ngano, badala yake wao kwa mawazo yao wenyewe na upofu wao wakamzania Yesu alikuwa anavunja sabato. Cha kushangaza roho ile ile iliyowaongoza Wayahudi, leo inawaongoza baadhi ya Wakristo kusema Yesu alivunja sabato, lakini Yesu Mwenyewe alisema wazi wazi kuwa hakuvunja sabato, na kwamba wanafunzi wake kuchuma masuke, na Yeye kuponya wagonjwa siku ya sabato ilikuwa ni halali wala si kuvunja Sabato, Akasema, “ni halali kutenda mema, na kuponya roho siku ya sabato” Marko 3:4. Lakini kwa sababu ya mioyo migumu na upofu wa Wayahudi, hawakuona kuwa Yesu alikuwa anafanya kilicho halali siku ya sabato, hivyo wakang’ang’ania kusema Yesu alivunja sabato.
Kwa maneno mengine kama ukisema Yesu alivunja sabato, inamaana utakuwa unasema wazi wazi kwamba Wayahudi walikuwa sawa kwa kumuhukumu Yesu kuwa amevunja sabato, na tena kama ukisema Yesu alivunja sabato, utakuwa unasema wazi wazi kabisa kwamba Yesu ni mwongo aliposema kuwa Yeye alifanya kitu ambacho ni halali kufanywa siku ya sabato, na hivyo hakuvunja sabato.
Tena kama ukisema Yesu alivunja sabato pale alipowaruhusu wanafunzi wake kuchuma masuke, au pale alipoponya wagonjwa siku ya sabato, utakuwa unasema wazi wazi kuwa si halali kutenda mema siku ya sabato. Na tena utakuwa unasema wazi kwamba Yesu alifanya dhambi, na hivyo utakuwa na sifa zilezile kama za Wayahudi wa zamani.
Wengine wanadai kuwa wanavunja sabato, kwa sababu Yesu aliivunja alipowaruhusu wanafunzi wake kuchuma masuke ya ngano, lakini Yesu mwenyewe alithibitisha kuwa hakuvunja, bali alifanya kilicho halali siku ya sabato, hivyo kama mtu akivunja sabato kwa sababu hiyo itamstahili hukumu; kwa maana Yesu hakuvunja sabato. Kama ukisema vinginevyo, utakuwa umesema wazi kuwa Yesu ni muongo!
…Fungu No. 8
Ufunuo 1:10 “Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,”
Baadhi wanasema wazi kwamba sabato ilibadilishwa kwa sababu ya neno “siku ya Bwana” lililotajwa hapo juu, wanadai kuwa siku ya Bwana ni siku aliyofufuka Yesu Jumapili. Lakini ukiangalia katika Maandiko utaona wazi kuwa ni waongo. Je siku ya Bwana ni siku gani kulingana na Biblia? Katika Isaya 58:13 Bwana Mwenyewe anasema, “Kama…ukiita sabato…siku takatifu ya Bwana…ndipo utakapojifrahisha katika BWANA…” Hapa Bwana Mwenyewe anaiita sabato ni siku takatifu ya Bwana. Kwa hakika Yesu Mwenyewe katika Agano Jipya alisema wazi kuwa “Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.” Mathayo 12:8. Hapa Yesu Mwenyewe anasema kuwa Yeye ndiye Bwana wa siku ya sabato. Siku ya Bwana ni sabato (Jumamosi).
Je unajua ni kwanini Jumapili wanaiita siku ya Bwana? Historia inasema…
“…kama sikukuu ya jua, Jumapili ilikuwa ni siku takatifu ya mungu Mithra; na inafurahisha kuona kwamba kwa sababu Mithra aliitwa Dominus, “Bwana,” Jumapili lazima ingekuwa ni ‘siku ya Bwana’ muda mrefu kabla ya Wakristo kuwepo.” -The Paganism in Our Christianity, Arthur Weigall, 1928, p 136
Neno “siku ya Bwana” katika Biblia linarejea siku ya sabato, ambayo Yesu Mwenyewe ni Bwana wa sabato. Lakini hata hivyo, wapagani wa zamani walilitumia kuiita Jumapili kama siku ya mungu wao Mithra. Mnamo mwaka 321BK wakati mfalme Constantine alipowataka Wakristo wote watunze Jumapili kitakatifu, aliita Jumapili “siku ya Bwana” wakati huo. Kanisa Katoliki lenyewe linakubali wazi wazi kuwa lilichukua mifumo hii ya kipagani na kuiingiza kanisani.
“Kanisa [Katoliki] lilichukua falsafa ya kipagani na kuifanya ngao ya imani dhidi ya mataifa. Lilichukua Pantheon ya kipagani ya Roma, hekalu la miungu yote, na kuifanya takatifu kwa mashahidi wote; hivyo inasimama hata leo. Lilichukua Jumapili ya kipagani na kuifanya Jumapili ya kikristo…Jua lilikuwa na watu wa kuliabudu wakati huo huko Persia na nchi zingine…Kwa hiyo kanisa lingeonekana kusema, ‘Tunza jina hilo la kipagani la zamani (Jumapili). Litabaki wakfu, na lililotakaswa.’ Na hivyo Jumapili ya kipagani iliyotolewa kwa Balder, ikawa Jumapili ya kikristo, takatifu kwa Yesu.” –William L. Gildea, “Paschale Gaudium,” katika Catholic World, 58, Machi, 1894, p. 809 [Katoliki wiki].
Leo wachungaji wengi wanadai kuwa Jumapili ni siku ya Bwana, kwa sababu Yesu alifufuka siku hiyo, lakini hawana hata fungu moja kwenye Biblia linalosema kuwa Jumapili ni siku ya Bwana, sababu wanazotumia ni mawazo yao tu wenyewe kusema kwamba wanaenda kanisani kila Jumapili siku ya Bwana, ili kuadhimisha ufufuo wake. Kama kweli wangelikuwa wanaenda Jumapili kanisani kuadhimisha ufufuo, kwanini hawaendi ijumaa kuadhimisha kifo pia? Je Ijuma siyo siku ambayo Yesu alikufa? Kitu ambacho wanachoshindwa kuelewa ni kwamba ufufuo wa Kristo hauadhimishwi kwa mtu kutembea kwenda kanisani Jumapili. Kifo na ufufuo wa Yesu vyote vinaadhimishwa kwa njia ya ubatizo pekee, wakati unapozamishwa majini, unaashiria kifo chake. Wakati unapoinuliwa kutoka ndani ya maji, unaashiria ufufuo wake.
Warumi 6:3-5 “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima. Kwa maana kama mlivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika mtaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake;”
Kama unadhani ukienda kanisani Jumapili ni kuadhimisha ufufuo wa Yesu, Jiulize Kuhusu hili; Mungu Mwenyewe hufanya kazi Jumapili, alipumzika akamuacha Mwanae kaburini siku ya Jumamosi, lakini Jumapili akamfufua.
Hebu niwaombe sana watumishi, omba sana Roho wa Mungu kabla hujaanza kufundisha manneo haya. Pia zipimeni kila Roho mnaposoma vitabu vyenu huko maana waandishi wengi na watumishi wengi sio wakweli leo, wengi ni waongo maana wana roho za mashetani kama ilivyo tabiriwa. Tuweni makini sana.
Mungu awabariki mno.
Dr. Samson.
Comments
Post a Comment